WANAWAKE wawili walioolewa katika familia moja ‘wake wenza’, mama Hashimu na mama Fadhila, wakazi wa Kimara King’ong’o jijini Dar, hivi karibuni walifikishwa serikali za mtaa kwa kosa la kutukanana matusi ya nguoni pamoja na kushikana uchawi.
Inadaiwa kuwa wanawake hao ‘walimwagiana’ matusi hayo usiku wa manane na kusababisha watu wengine kukosa usingizi na kukusanyika kuwasikiliza.
Mara baada ya kufikishwa serikali ya mtaa, wake wenza hao walitakiwa kueleza ugomvi wao na kila mmoja kuanza kushusha tuhuma kwa mwenzake.
Mapaparazi wetu waliwashuhudia wakati wake wenza hao walipokuwa wakijieleza mbele ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa King’ong’o, Demetrius Mapesi na Mtendaji wake Amina Rashid.
Mama Hashimu alianza kuelezea kisa kizima na kufuatiwa na mama Fadhila ambaye wakati akijieleza alipandisha mori kiasi cha kumfanya atake kumrukia mwenzake.
Unajua nasikia hasira sana kwa sababu mama Fadhila ameniita mchawi huko mtaani unadhani mimi nitaelewekaje? Ukweli kauli hiyo inaniuma sana,” alisema mama Hashim na kuangua kilio.
Hata hivyo, baada ya kila mmoja kueleza ya moyoni, mwenyekiti wa serikali za mtaa pamoja na mtendaji wake, waliwaamuru wake wenza hao kupeana mkono na kuombana msamaha. 

“Sasa hapa hakuna kesi, kwani wote mna makosa, hebu niambieni mnawafundisha nini watoto wetu kwa matusi
mliyotukanana hadharani?” alihoji mwenyekiti na kuwataka wayamalize mambo hayo.
Aidha, mwenyekiti huyo aliahidi kuwafuatilia ili kuona kama watakuwa wamebadili tabia zao.
Kama vile haitoshi aliwaahidi kama watarudia atawahamisha mtaa pamoja na waume zao kwani mtaani kwao hawahitaji watu wanaotukanana ovyo na kuzushiana mambo ya kichawi.
Baada ya tamko la mwenyekiti, mtendaji wake aliwaamuru wake wenza hao kuandika matusi waliyotukanana kisha akawapiga faini ya shilingi 20,000 kila mmoja.
“Kutokana na matusi yenu nalazimika kuwapiga faini ya shilingi elfu ishirini kila mmoja, ingawaje kwa mujibu wa sheria ya Tanzania mtu akikutwa na hatia ya kutukana anatakiwa kutozwa faini ya shilingi elfu hamsini au kufungwa jela miezi sita,” alisema mtendaji huyo.
Kila mmoja alilipa nusu ya faini na kuahidi kumalizia huku wakisema kuwa hawatarudia kufanya kosa hilo tena
 
Top