Mwenyekiti
wa mtaa wa Lulumba New Kiomboi mjini wilaya ya Iramba, Abel Seit akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya tukio la
mtoto wa kike Zuhura (6) kumwagiwa maji ya moto na bibi yake Magreth
Sombi (55) na kusababisha kifo chake.
Mwenyekiti
wa mtaa wa Lulumba New Kiomboi mjini wilaya ya Iramba,Abel Seit
akifungua mlango wa nyumba ya Magreth Sombi ambaye kwa sasa anashikiliwa
na polisi kwa tuhuma ya kumuuguza mjukuu wake Zuhura na kusababisha
kifo chake.
Sehemu ya ndani ya nyumba ya mtuhumiwa Magreth Sombi anayedaiwa kumuuguza mjukuu wake maji ya moto na kusababisha kifo chake.
Picha
na mtoto wa mtuhumiwa Magreth Sombi,Naomi ambaye hivi karibuni
amehitimu mafunzo ya ualimu mkoani Tabora na alikuwa anasubiri kupangwa
kazi.Kwa sasa Naomi na mama yake Magreth Sombi wanashikiliwa na jeshi la
polisi wilaya ya Iramba kuhusiana na mauaji ya Zuhura.
Picha
ya mtuhumiwa Magreth Sombi anayetuhumiwa kumuua mjukuu wake Zuhura kwa
kumumwagia maji ya moto ambayo yaliyokuwa yatumike kupikia ugali wa
jioni.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Kiomboi
Mtoto
wa kike aliyetambulika kwa jina moja la Zuhura (6) mkazi wa mtaa wa
Lulumba New Kiomboi mjini, wilayani Iramba,amefariki dunia baada ya
kudaiwa kuuguzwa kwa maji ya moto na bibi yake Magreth Sombi (55).
Imedaiwa
kwamba Zuhura alimwagiwa maji ya moto ambayo yalikuwa yatumike kupikia
ugali,kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kitendo cha mtoto huyo kuchelewa
kukabidhi mwiko aliotumwa na bibi yake.
Akisimulia
mkasa huo wa aina yake,Mwenyekiti wa mtaa wa Lulumba,Abel Seit,amesema
tukio hilo limetokea Septemba 24 mwaka huu majira ya jioni huko mtaa wa
Lulumba katika mji wa New Kiomboi.
Amesema
siku ya tukio,Zuhura alitumwa na bibi yake Magreth akalete mwiko wa
kusoga ugali wa jioni na inadaiwa kwamba mtoto huyo alichelewa
kuukabidhi mwiko huo.
Seit amesema baada ya kuleta mwiko huo,alimwagiwa mwilini maji yaliyokuwa yamechemka tayari kwa kutumika kupikia ugali wa jioni.
“Kama
vile adhabu hiyo haikutosha,Magreth kwa ushirikiano na mtoto wake
Naomi,walimkamata kwa nguvu Zuhura na kisha kuingiza viganja vyake vya
mikono yote ndani ya sufuria iliyokuwa ina maji yaliyokuwa yamechemka
kwa kiwango cha juu.Mtoto Zuhura aliweza kuugua na nyama zote kutoka na
kubakia mifupa”amesema kwa masikitiko mwenyekiti huyo.
Seit amesema Zuhura alifariki dunia Septemba 25 akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Iramba.
“Baada
ya muda mrefu kupita baada ya Zuhura kufariki dunia,bibi yake Magreth
alimtuma mtoto wake Naomi kuja nyumbani kwangu kunipa taarifa hiyo.Cha
ajabu ni kwamba hawakupiga yowe wala kutoa taarifa kwa majirani
zao”,amesema na kuongeza;
“Nilipomhoji
ni kwa nini hajawajulisha majirani zao juu ya kifo hicho,kwanza
alinionya kwamba nisije nikawaambia watu wala majirani kwa sababu hataki
watu wajue au waje warundikane kwake na kwamba mwili wa Zuhura wakati
wo wote utachukuliwa na wazazi wake kwenda kuzika Singida mjini”.
Kwa
upande wake jirani wa karibu wa Magreth,Elieza Mgwali,amesema Zuhura
ambaye ana miezi miwli toka aanze kuishi na bibi yake,aliishi kwa mateso
makubwa.
“Mtoto
huyu ameteseka mno toka aanze kuishi na bibi yake,alifanyishwa kazi
ambazo ziko nje ya uwezo wake na mara nyingi alikuwa akinyimwa hata
chakula.Mara nyingi tu tulikuwa tunashitukia anaingia kwetu na kwenda
moja kwa moja jikoni na kujichukulia chakula bila hata kuomba.Kwa sababu
tuliisha tambua mateso yake,tulikuwa tukimruhusu ale hadi
ashibe”,alisema.
Majirani
wa Magreth wamepigwa butwaa kutokana na kitendo hicho kufanywa na mama
ambaye alikuwa hakosi kanisani na alikuwa mwimbaji mzuri wa kwaya.”Kumbe
chui aliyekuwa amevaa ngozi ya kondoo”,alisikika mama mmoja ambaye
alidai kuwa walikuwa wakisali na Magreth.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa,Magreth na mtoto wake Naomi,wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.
Juhudi
kubwa zimefanywa na mwandishi wa habari hii kupata undani wa mauaji
hayo,hazijaa matunda baada ya kumpigia Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida
kupitia namba yake ya simu ya mkononi kuita bila kupokelewa na hata
meseji ilipotumwa nayo haikuweza kujibiwa.