Balozi huyo alisimama jukwaani takribani wiki mbili zilizopita katika moja ya mikutano iliyohutubiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, katika wilaya za Kishapu na Shinyanga Mjini.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uwekaji saini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Baraza la Wafanyabiashara wa watu wa China Tanzania (CBCT).
Alisema alikwenda mkoani Shinyanga kwa shughuli za kiserikali kuwahamasisha wananchi wa mkoa huo kulima zaidi pamba na siyo mwaliko wa CCM kama inavyotafsiriwa na baadhi ya watu.
Balozi Youqing alisema alipokuwa katika mkutano huo wilayani Kishapu, alipewa nafasi ya kuwasalimia wananchi wa mkoa huo na kuwahamasisha juu ya ulimaji wa pamba.
Alisema mara baada ya kupanda jukwaani ghafla alitokea msichana asiyemfahamu wala kumkumbuka aliyemvua kofia yake na kumvika ya CCM kwa nguvu.
Alieleza kuwa alijaribu kumzuia msichana huyo, lakini alishindwa.
“Alikuja msichana mmoja mrembo, ghafla wakati nikiwa jukwaani, nilijaribu kumzuia kunivua kofia yangu, lakini nilishindwa, alitumia nguvu,” alisema Youqing.
Alisema hakuna mtu yeyote hapa nchini atakayeweza kumzuia balozi wa China kufanya vitu vizuri vyenye faida kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Alisema hakujua kama kitendo kile kingetafsiriwa vibaya na wananchi wa Tanzania, na kueleza kuwa hakujua kama Watanzania wangekasirika kwa kuwa anaamini Watanzania wote ni kitu kimoja. Balozi huyo alisema yupo tayari kufanya kazi na chama chochote cha siasa nchini alimradi sheria na taratibu zifuatwe.
Hatua ya balozi huyo kuvaa kofia ya CCM ililalamikiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Septemba 16, mwaka huu kupitia kwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Ezekia Wenje, aliyesema kitendo cha Balozi Youqing kilikiuka mkataba wa Vienna wa mwaka 1961.
Wenje alisema kuwa kutokana na hali hiyo, Chadema kitaiandikia Serikali ya Tanzania, Umoja wa Mataifa na Serikali ya China kuwasilisha malalamiko dhidi ya Balozi Youqing.
Chama hicho kiliongeza kuwa kisingependa uhusiano wa kihistoria kati ya China na Tanzania ambao umedumu kwa muda mrefu tangu Uhuru uingizwe matatani au shakani kwa sababu ya mapenzi binafsi ya balozi kwa CCM.
Siku hiyo hiyo, Septemba 16, mwaka huu, serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ilisema kuwa kitendo kilichofanywa na Balozi huyo siyo sahihi na kinakiuka mkataba wa Vienna.
Membe alisema kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia.
Taarifa ya Waziri Membe ilieleza kuwa mkataba huo unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na ushabiki wa kisiasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki na kwamba kwa tukio hilo la Balozi wa China, Wizara itachukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hilo lisitokee tena.
Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Alhamisi iliyopita alikemea kitendo cha CCM kumshirikisha Balozi Youqing, katika shughuli zake za kisiasa.
Alisema tukio hilo ambalo CCM kiliruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake, ni dhahiri limezua hali ya taharuki kwa wananchi na kwamba Sheria ya vyama vya Siasa kwa upande wake iko kimya katika suala hilo.
Jaji Mutungi alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inaunga mkono kwa dhati kabisa hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea jambo hilo na kwamba tamko la serikali limezingatia sheria na wajibu wa wanadiplomasia wakati wa uwapo wao nchini.
Jaji Mutungi alisema kama mlezi wa vyama vya siasa, anavitaka vyama hivyo kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
Alisema kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa sasa ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya Sheria husika ya Vyama vya Siasa ambayo imebainika kuwa na upungufu na lengo ni kukabiliana na changamoto zilizopo ikiwamo suala hili lililojitokeza.
AZUNGUMZIA WACHINA KUTISHWA
Katika hatua nyingine, Balozi Youqing alizungumzia madai ya kuandikiwa barua na Mtanzania mmoja anayejitambulisha kama Kamanda wa CCM Asilia alitaka Wachina wote waondoke nchini kabla ya kuanza kuuawa kutokana na balozi wao kushabikia CCM na Wachina kujihusisha na uhalifu, na kusema kuwa anaamini Tanzania ina sheria na taratibu zinazozuia mtu kuvunja sheria.
Hivyo kama kuna atakayebainika kufanya kitendo hicho, sheria itachukua mkondo wake.
Alisema kitendo chochote cha uvunjifu wa amani kinachoweza kutokea hapa nchini anaamini Jeshi la Polisi litapambana nalo. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, alipotafutwa kuelezea tukio hilo la raia wa China kutishiwa kuuawa, alisema Polisi bado wanachunguza.
“Vijana wangu bado wanafuatilia hilo suala, wapo kazini,” alisema Manumba.