Eurasian, Georgia. Katika baadhi ya tamaduni siyo ajabu kusikia kwamba mama amemtunza mwanaye kwa kipindi cha miaka 40, lakini inashangaza ikiwa atamtunza akiwa amekufa kwa miongo miwili.

Baada ya John Barakaradze kufariki akiwa na umri wa miaka 22, familia yake inayoishi Mji wa Eurasian nchini Georgia haikumzika kijana wao tofauti na ilivyo kawaida ya mtu anayekufa kuzikwa, badala yake iliamua kumhifadhi kwa miaka 18.

Mama wa John, Tsiuri Kvaratkhelia aliliambia Shirika la Habari la Georgia kuwa aliamua kuhifadhi maiti ya mtoto wake, ili mjukuu wake akikua aweze kuona maiti ya baba yake. “Nilimhifadhi ili mjukuu aone baba yake alikuwaje,” alisema Tsiuri.

 Mwili wa Bakaradze ulihifadhiwa katika jeneza maalumu na kwa aliyehitaji kumwona, aliweza kumwangalia kupitia dirisha maalumu. Kvaratskhelia aliliambia shirika hilo kuwa familia yake ilianza kutumia njia za jadi ikiwamo pombe kali ili kuhifadhi mwili huo. Alieleza kuwa katika shughuli hiyo ya kuhifadhi mwili, walipambana na mambo mengi ikiwemo matukio ya ushirikina ambapo mara kwa mara alikuwa akiota ndoto iliyomweleza kuwa aachane na matumizi ya dawa za kienyeji, badala yake aweke pombe aliyoitaja kwa jina ili kuutunza mwili huo.

“Niliwahi kuota ndoto. Kuna mtu aliniambia kwenye ndoto niamke na nianze kutumia pombe kali ili kuutunza mwili huo,” alisema Kvaratskhelia katika mahojiano hayo.

Aliongeza: “Tangu hapo nilianza kutumia na sasa miaka mingi imepita. Niliambiwa kwamba nisiache, kila siku usiku niweke pombe hiyo la sivyo maiti ya mwanangu itageuka na kuwa nyeusi.”
 
Top