Roxanne Allen.
Mwanamke mmoja ambaye aliuza kila kitu chake katika mnada wa hadhara ili kuweza kugharimia mazishi yake, amefariki dunia juzi asubuhi.

Roxanne Allen mwenye miaka 51 kutoka Ozark, Missouri aligundulika kuwa na saratani mnamo Mei 2011.
Julai mwaka huu, madaktari walisema saratani yake ilikuwa imefikia hatua za mwisho na kwamba alikuwa na wiki chache tu za kuishi.
Hivyo aliamua kutumia siku zake chache za mwisho kuisaidia familia yake kwa kuchangisha kiasi cha pesa cha kutosha kugharimia gharama za msiba wake.
Kupata kiasi hicho aliandaa mnada wa hadhara Julai na kuuza vitu vyake vyote anavyomiliki - kuanzia nguo za watoto hadi samani.
"Ninalazimika kufanya hivi kwa ajili ya mama yangu," alisema.
"Na nina vitu vyote hivi kwa ajili ya kuuza ambavyo vitasaidia kugharimia msiba wangu. Na sikutaka kuacha uchafu wote huu ili mama yangu asafishe. Au watoto wangu."
"Hii ni zawadi ya kipekee, kubwa kuliko zote, kwa kile alichotaka kufanya mwenyewe na sio mimi kuhofia siku itakapofika," mama yake, Shirley Waddell, alisema.
Lakini haikuwa rahisi kutazama vitu alivyokuwa akimiliki maishani mwake vikiuzwa.
"Nilimwona akibubujikwa machozi baada ya kipindi kirefu pale alipotazama kitu ambacho kilivuta hisia kiasi fulani au thamani kubwa na kutazama mtu fulani akiondoka nacho," alisema mchumba wake, Daniel Beckett.
Wawili hao walikuwa wamepanga kuoana, lakini pale Allen alipogundulika kuwa na saratani akabadilika na kuwa mbinafsi na kuamua kutoendelea na mipango hiyo. Alimweleza Beckett kwamba hakuwa akitaka kumfanya mgane.
Baada ya kusikia habari yake, kampuni inayohusika na misiba ya Fraker Funeral Home ya huko Marshfield ikakubali kulipia gharama zote za msiba wake.
 
Top