TUKIO kubwa la kigaidi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika jengo la maduka makubwa na ya bei mbaya jijini Nairobi la Westgate, limeelezwa kuwa liliongozwa na mwanamke raia wa Uingereza, Samantha Lewthwaite.
Yafuatayo ni mambo kumi usiyoyajua juu yake.

1. Samantha, mwenye umri wa miaka 29, ni mzaliwa wa Buckinghamshire, Uingereza anayeelezewa na magaidi wa kundi la Al Shabaab kama mwanamke mwenye akili nyingi, akiwa ni mama wa watoto watatu ambaye alikata mawasiliano na familia yake baada ya kuhamia Kenya mwaka 2007.
2. Ripoti za kipolisi zinaonesha kuwa ni mkufunzi wa wanawake wa kikundi hicho cha kigaidi wanaochukua mafunzo ya jihad, mke wa zamani wa Germaine Lindsay, ambaye alijiua baada ya kuhusika na shambulio la bomu kwenye treni ya chini ya ardhi jijini London, Julai 7, 2005.
3. Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zinazoaminika kuwa ni zake, ambazo zilitangazwa na Gazeti la Daily Mail la Uingereza, mwanamke huyo anawalea watoto wake ili waje kuwa wanaharakati wa imani kali. Mumewe wa pili, Habib Saleh Ghani naye ilidaiwa kuwa aliuawa kwenye tukio lingine la ugaidi.
4. Baadhi ya nyaraka zinaonesha kuwa katika baadhi ya mawasiliano na mumewe, aliwahi kusema: “Ghani alizungumza na kijana wangu wa miaka nane na binti yangu wa miaka mitano akiwauliza wanachotaka kuja kufanya wakiwa wakubwa, wana majibu mengi lakini wote wanakubaliana kwamba watakuja kuwa Mujahidina.
5.  Ni mtaalamu wa kutengeneza vifaa vya kuficha sura, pua na kichwa, akiachana na taaluma yake ya zamani ya ubunifu wa mitindo ya mavazi ambayo sasa anashona yanayovaliwa na Waislamu, kazi aliyoianza akiwa chini ya uangalizi wa magaidi hao wakati akiishi Mombasa nchini Kenya.
6. Anahisiwa kuwa ndiye aliyetupa guruneti katika baa iliyokuwa imejaa mashabiki wa soka wakitazama mechi za Euro mwaka 2012 katika mechi kati ya England na Italia nchini Uganda Juni 24 na kuua watu watatu, akiwemo mtoto aliyekuwa na umri wa miaka mitatu. Isack Simiyu, (23), aliyekuwa nje ya Jericho Bar, alisema shambulio hilo lilifanywa na mwanamke wa kizungu aliyejifunga kitambaa cheusi kichwani. Alidai kumuona vizuri mlipuaji huyo na polisi walipompa picha nne za wanawake wa kizungu ili aone kama mlipuaji alikuwa mmojawapo, aliichagua ya Samantha.
7. Ni gaidi wa kike anayetisha zaidi kwa sasa tokea alipoondoka Ulrike Meinhof, mwanzilishi wa Kundi la Red Army ambalo lilihusika na milipuko ya mabomu katika Ujerumani Magharibi kwenye miaka ya 1970.
8. Alipokimbia katika nyumba aliyokuwa amepanga mjini Mombasa, polisi walikuta kitabu kidogo cha kumbukumbu akiwa ameandika kuwa anataka watoto wake waje kuwa wakujitoa mhanga. Pia walikuwa na bunduki za kisasa, risasi, pamoja na mapipa ya kemikali yanayotumiwa na wanaojilipua.
9. Akiwa na jina la Kiislamu la Asmaa Shahidah Bint-Andrews, kijana wake wa kiume, Abdur-Rahman Faheem Jamal, alizaliwa katika Hospitali ya Stoke Mandeville mwaka 2009. Katika cheti cha kuzaliwa cha mwanae, hakuna jina la baba lililoandikwa. Alislimu akiwa na miaka 18, akiachana na uvaaji wa jeans na Tisheti na badala yake akivaa mavazi ya Kiislamu, ikiwemo hijab.
10. Alisoma masomo ya dini na siasa katika shule iitwayo Oriental and African Studies huko Russell Square, London, umbali wa mtupo wa jiwe kutoka pale mumewe alipojiua kwa kujilipua.
 
Top